BINAFSI
WATU wengi hudhani kulipiza kisasi au kumtendea ubaya aliyekutendea ubaya ndio jambo linalofaa. Jaribu kutolipiza kisasi na umtendee wema aliyekutendea ubaya. Lazima lipo litakalokushangaza tu.
NYUMBANI
ISRAFU ni matumizi mabaya kwa kile mnachoruzukiwa na aliyewaumba. Wafundishe jamaa yako 'uchumi' katika matumizi. Ziada inayozidi inaweza ikatolewa kwa wahitaji kwa baraka zaidi kwa familia yenu. Israfu ikiendelea bila kudhibitiwa hujenga familia isiyojali na isiyo na huruma.
NJIANI
KUWA mwangalifu na waendesha baiskeli na vijana wenye magurudumu miguuni. Tahadhari inahitajika sio tu kujihami mwenyewe bali pia kukuepusha wewe kuwa chanzo cha umauti au ulemavu kwa hao wapanda baiskeli na waburuza 'rolasketi' .
SAFARINI
SAFARINI huweza kugeuzwa sadaka au ibada ya aina fulani. Ukisafiri jenga mazoea ya kuulizia ndugu, jamaa au Watanzania wenzako wanapoishi. Kwalo hilo unaweza kupeleka faraja kwa wenye dhiki au maradhi. Na kama sehemu unaijua ni vizuri pia kutembelea hospitali za karibu. Afya yako ya mwili na akili yaweza kuimarika kwa hili.
KAZINI
MAHALA pa kazi huweza kugeuzwa kituo kizuri cha upatu au SACCOS jinsi mnavyotaka wenyewe. Ili mradi tu kuchagua watu waaminifu kusimamia shughuli yenyewe. Kuchanga shilingi elfu moja au mbili kwa wiki kunaweza kuja kukusaidia katika shida usiyotegemea.
SHULENI
KUSOMA sana sio kufaulu sana. Watazame wanaobukua usiku na mchana ulinganishe na matokeo yao bila shaka utawasikitikia. Kusoma kunahitaji kuweka mikakati na kutumia akili zaidi ya darasani.
NCHI ZA NJE
KAZI nyingine za nje ni kuwa boi au yaya nyumbani kwa mtu. Tofauti na hapa Tanzania ni ule ukweli kuwa mshahara ni mzuri na unaweza ukatuma fedha nyumbani. Ili mradi upate mwajiri anayemwogopa Mungu. Vinginevyo unaweza kunyanyasika huko kiasi cha kutisha. Chunguza kwanza kabla ya kuamua.
BURUDANI
Mchezo wa kurusha vishale (darts) ni burudani kwa watu wanaopenda starehe ya mchezo wa kikundi. Katika burudani hii unaweza kuzungumza na marafiki na jamaa; unaweza kunywa na mnaweza mkapanga mambo mbali mbali ya kufanya siku zijazo. Ni burudani inayochochea uvumbuzi, uzuzi na ujasiriamali.
MICHEZONI
WANAOHARIBU michezo wakati mwingine ni waandishi wa habari na vyombo vyao. Hivi sasa baadhi yao wanafundisha kuliko kocha, wanacheza kuliko mchezaji bora; na ni waamuzi wa kutegemea kuliko waamuzi wa mechi husika. Hili halisaidii michezo. Linabomoa michezo.
MJINI
KATIKA miji yetu mingi hivi sasa jenga mazoea ya kutazama mguu wako unakotua. Katika baadhi ya mitaa usipofanya hivyo utajikuta umetumbukia kwenye shimo bila kutarajia.
Kwingineko unaweza kukanyaga kinyesi au kitu kinachoweza kukudhuru. Aidha baiskeli, mikokoteni na magari yako huru kupita hata unakojificha.
VIJIJINI
UMASIKINI kwa wakazi wa maeneo pembeni ya bahari ni wa kujitakia ? Pengine. Kuna hoteli ya Mzungu huko Saadani imejengwa kwa makuti, majamvi na mkeka. Kila kinachotumika hotelini kinatengenezwa au kulimwa au kuvuliwa na wanakijiji wenyewe. Amkeni mlio kando ya bahari mnaweza kuwa wamiliki wa hoteli za kitalii eti!
Barua-pepe: ishi.jamboleo@gmail.com
Monday, November 30, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment