Monday, November 30, 2009

ishi - Desemba 1, 2009

BINAFSI

NAFSI inasemekana iko katika daraja tatu. Daraja la chini kabisa ni la nafsi
inayojifikiria yenyewe daima na kutaka kujitosheleza mara moja kwa lolote lile.
Nafsi ya pili ni ile inayojua sio rahisi kujitosheleza mara moja nyakati zote. Na
ile ya juu kabisa ni ile inayojua kusimamia nafsi ya kwanza na ya pili ili
mustakabali wa mtu binafsi sikuzote uwe bora.
*******************************************************************************

NYUMBANI

NYUMBA mnayoishi ndiyo Ikulu ya wanafamilia. Heshima yake lazima iwe juu ya heshima kwa sehemu nyingine yoyote. Hapa ndio kimbilio la wote kwa yote wanayokutana nayo katika shughuli zao za maisha ya kila siku. Amani na utulivu ni muhimu kutawala mahala hapa. Isipokuwa hivyo sio rahisi kwa anayetoka nyumba hiyo kufanikiwa katika lolote lile.
*********************************************************************************

NJIANI

NJIA ni mapito ya kila mtu. Haifai kwa yeyote yule kudhani au kutenda jambo
linaloonesha kana kwamba njia ni yake na mwenzie tu. Onyesha utu na tumia busara unapokuwa njiani kuwaachia watu wengine nao nafasi ya kuitumia kama wewe usivyopendwa kukwazwa na mtumia njia mwingine.
*********************************************************************************

SAFARINI

UNAPOKUWA safarini ni vizuri kufahamiana na msafiri au wasafiri wenzako. Tendo hili huwa gumu kwa wengine hadi pale wanapopatwa na shida fulani. Usingoje shida kukufikandiyo umjue msafiri mwenzio. Busara na hekima zinaonesha wanaowasalimia wasafiri wenzao hata wale wasiowajua huwa na safari njema na bora zaidi.
********************************************************************************

SHULENI

Shuleni ni mahala pa kuafuta elimu. Sio mahala pa kujionesha au pa kushughulika na yale yasiyochangia lolote kuoneza elimu au maarifa yako. Upo ushahidi wa kutosha kwamba wale wanaofika shuleni kwa malengo mengine badala ya yale yaliyokusudiwa, yaani, kuelimika, huwa na wakati mgumu shuleni.
********************************************************************************

KAZINI

KAZI yoyote ile ni mkataba wa hiari kati ya mtoa ajira na mwajiriwa. Kabla hujafanya maamuzi ya kuwa mwajiriwa wa sehemu fulani hakikisha kwamba maslahi na matarajio yako yatafikiwa kwa kukubali kuajiriwa na mwajiriwa fulani. Vinginevyo huko mbele ya safari utakapoona maslahi yako ni duni na matarajio yako mengi ni njozi utajidhalilisha mwenyewe na yule aliyekuajiri.
*******************************************************************************

NCHI ZA NJE

UKIWA nchi za nje ni vizuri utumie siku zako za kwanza kuwajua wenyeji wako na mazingira yako. Hata kabla hujaondoka kwenu ni vizuri upate habari za kule
unakokwenda. Hili litakusaidia kupata mwanga wa tabia na mienendo ya wenyeji wako. Vinginevyo unaweza kujikuta mengi yanakuharibikia kwa kuwa tu hujawajua wenyeji wako na mazingira yako ipasavyo.
********************************************************************************

BURUDANI

BURUDANI ya kweli sio lazima iwe inayotumia fedha. Burudani ni jambo lolote lile linalokutoa katika mazingira ya mihemuko na shiniko za kazi au shughuli za kawaida na kukupeleka mahala kwenye utulivu au msisimko fulani unaokukurubisha wewe na mazingira yako au yule au wale uwapendao na hivyo kupata fursa ya kuibwaga chini mizigo ya maisha unayoibeba kila siku katika siku zako za kazi, masomo au shughuli nyingine yoyote ile iwayo.
********************************************************************************

MICHEZONI

MICHEZO huanza kwa kuwa na sehemu ya michezo. Jamii inayoshindwa kuwa na sehemu ya michezo ni jamii ya kishenzi na iliyo nyuma sana kimaendeleo. Wahenga walituambia kuwa malezi ya watoto na vijana bila shughuli za kuwapotezea muda ni kitu kigumu na chenye hatari ya kuingiliwa na shetani wakati wowote ule. Tuajribu kuhimiza kuwepo kwa viwanja vya michezo kwa kila kata kama sio mtaa kote nchini.
********************************************************************************

MJINI

MJINI ni sehemu ambayo imani, amani, wema, ukarimu na ucha Mungu huwa mdogo sana kwa sababu ya ushindani, wivu, kuiga, tamaa na watu kutaka kujionesha.

Maisha bora hayapatikani kwa kuiga wengine na kutaka kuwa wao. Maisha bora
hupatikana kwa wewe kuwa kile unachostahili kuwa na sio vinginevyo. Muigaji siku zote ni nyani. Mwenye lake la asili hata kama sio bora wala zuri sana ana heshima mara kadhaa kuliko mwigizaji wa kile anachodhani ni bora na zuri zaidi. Turingie kilicho chetu, turingie asili yetu.
********************************************************************************

VIJIJINI

MAISHA ya mjini ni ya mwendo mdebwedo na ndivyo yanavyostahili kuwa. Ni heri kwako kwenda nao kuliko wewe kutaka waige mwendo wako wa mjini na wa kimaendeleo.

Katika hili kuna sili ya asili na fasili. Polepole ya mwanakijiji ndio mwendo wa
asili wa binadamu. Haraka haraka ya mjini ni kielelezo ya jitihada kama zile za mbio za farasi sakafuni.

********************************************************************************

No comments:

Post a Comment